KATIKA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA
DIVISHENI YA KAZI
MUSOMA MJINI
MAOMBI YA MAREJEO NA 23 YA 2020
BAINA YA
NORTH MARA GOLD MINE LTD__________________ MUOMBAJI
VERSUS
GERALD NZUMBI____________________________ MJIBU MAOMBI
(YaHyotokana na uamuzi wa Tume ya Usuiuhishi na Uamuzi iiiyokaa Musoma mjini, Mheshimiwa Kadeha Muamuzi, katika mgogoro wa kazi na. CMA/MUS/334/2019 uiiotoiewa mnamo tarehe 30. 07. 2020)
HUKUMU
Tarehe 4 & 22 Januari 2021
GALEBA, J.
Katika maombi haya, muombaji North Mara Gold Mine Ltd ni kampuni ya kitanzania na mjibu maombi ni mtanzania. Muombaji ana makao rasmi Tan House Tower, Ursino Kusini Barabara ya Bagamoyo Dar es Salaam na mjibu maombi ni mkazi wa mkoa wa Tabora kwa mujibu wa mkataba wake. Kwa sababu hii na nyingine kadhaa kama itakavyooneshwa hapa chini, hukumu hii imeandaliwa kwa Kiswahili ila itakapolazimu sana ndipo lugha za Kiingereza au Kilatini zitatumika. Ikumbukwe kuwa kwa mahakama kutoa hukumu kwa Lugha ya Taifa hapa nchini siyo jambo lisilo la kawaida wala geni au la mara ya kwanza. Kwa mfano, kwanza, iliyokuwa Mahakama ya Kazi ilikuwa ikitoa hukumu zake kwa Kiswahili na kuzichapisha kwenye gazeti rasmi la Serikali, pili, Mahakama zote za Mwanzo 960 nchini tangu kuanzishwa kwake hutoa maamuzi yake ya kisheria kwa Kiswahilili na tatu, mabaraza yote ya kata zaidi ya 3, 900 Tanzania bara hutoa maamuzi yake yanayoheshimika na yenye nguvu za kisheria kwa lugha ya Kiswahili. Kadhalika, hoja za mawakili au wadaawa mbele ya mahakama zote nchini kuanzia mahakama za mwanzo mpaka Mahakama ya Rufaa kwa kiasi kikubwa hutolewa kwa Kiswahili. Ni uchukuaji tu wa kumbukumbu na uandishi wa hukumu za mahakama za wilaya, hakimu mkazi, mahakama kuu na Mahakama ya Rufaa hulazimika kuandikwa kwa Kiingereza kwa mujibu wa sheria.
Ni hoja ya mahakama hii kwamba ili kuimarisha zaidi nguzo ya Utawala wa Sheria ijulikanayo kama Kuifikia Haki au Upatikanaji wa Haki au Acccess to Justice, ni muhimu kutumia Lugha ya Taifa katika utunzaji wa kumbukumbu za kimahakama na hukumu za mahakama zote kwa lugha hiyo, ambayo ndiyo hasa lugha ya wananchi walio wengi. Bila shaka, hoja hiyo haiondoi haki za watu wengine kama vile waingereza wenyewe au wageni kutoka ng'ambo au hata kwa matakwa ya wadaawa wenyewe kama wakipendelea kitumike Kiingereza katika shauri lao. Miaka michache iliyopita, katika kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa haraka na bila vikwazo visivyo vya msingi, Mahakama ya Tanzania iliondoa malipo kwa wananchi kulipia nakala za hukumu; lakini bado mwananchi akipewa hiyo hukumu hata kama hakulipishwa mahakamani, ni lazima tena atafute fedha za kumlipa wakili au msomi mwingine anayejua lugha hiyo ya kigeni ili aweze kumsomea na kumtafsiria ili aweze kuelewa ni nini hasa hukumu inazungumzia. Kwa lugha rahisi ni hivi, pamoja na mwananchi kumuondolea gharama ya kulipia hukumu mahakamani ili kupata nakala ya hukumu, bado ana gharama nyingine ya kulipia kabla ya kuelewa kilichoandikwa kwenye hukumu aliyopewa mahakamani.
Kifungu cha 4(1)(c) cha sheria ya Baraza la Kiswahili la Taifa
Sura ya 52 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kinasema hivi;
4 (1) The functions of the Council shall be-
- N/A
- N/A
- to encourage the use of the Kiswahiii language in the conduct of official business and public life generally;
Kifungu hicho kidogo kinaweza kutafsiriwa kama ifuatavyo;
'4 (1) Majukumu ya Baraza la Kiswahili yatakuwa ni-
- (hakihusiki)
- (hakihusiki)
- kuhimiza matumizi ya Kiswahiii katika shughuii rasmi za kiserikaii na za umma kwa ujumla wake; '
Kwa maana nyingine, mwaka 1967 wakati sheria hiyo ilipotungwa Bunge liliona kuna umuhimu wa kuweka chombo cha kitaifa yaani Baraza la Kiswahili la Taifa kwa ajili ya kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli zote rasmi za kiserikali na za umma. Ni hoja ya mahakama hii kwamba utoaji haki ni jambo rasmi, la kiserikali na la umma ila sasa ni miaka 54 tangu tuanze kuhimizwa kutumia Kiswahili katika shughuli hizo lakini kwa mahakama bado, haijaruhusiwa na sheria kutumia Kiswahili.
Japokuwa hili jambo (la matumizi ya Kiswahili kuandika hukumu za kimahakama) halina uhusiano na hoja za pande mbili katika maombi haya, yaani ni "obita dictum" ila ni rai ya mahakama hii kwamba Bunge liangalie namna ya kuisaidia Mahakama kuweza kueleweka kwa urahisi zaidi kwa wananchi inaowatumikia kwa kufuta sheria zinazoishurutisha kutunza kumbukumbu zake na kuandika hukumu kwa Kiingereza wakati wananchi walio wengi Kiingereza hawakijui kabisa au hawakijua kwa ufasaha.
Sisi mahakamani wakati wote tunajua kwamba kwa Ibara za 4(2), 107A na 107B za Katiba ya Nchi, jukumu tulilonalo la awali na la msingi kabisa ni kutoa huduma ya utoaji haki kwa wananchi wa nchi ya Tanzania.
Kwetu sisi lengo ni wananchi; kwa ajili ya watu wengine wasiojua Kiswahili ili waweze kuzielewa hukumu zetu, kunaweza kukawa na utaratibu wa kutafsiri kila hukumu inayotoka, lakini lengo la uwepo wa Mahakama ya Tanzania ni kutauta migogoro ya wananchi. Ni shauku ya mahakama hii pia kwamba ikitoa hukumu ikampa mwananchi nakala, mwananchi huyo asome hiyo hukumu mwenyewe na aelewe vizuri kwa lugha yake mwenyewe mahakama ilivyotatua mgogoro baina yake na upande mwingine. Kwetu sisi hilo jambo litakuwa ni la fahari na la fanaka.
Vyovyote vile, katika maombi haya napata faraja, nguvu na mamlaka ya kisheria kuandika hukumu hii kwa Lugha ya Taifa kutokana na Kanuni ya 4(1) na (2) za Labour Court Rules 2007, GN 106 of 2007 inayotamka wazi kwamba;
'4(1)The language of the Court shall be bi-lingual in either Engiish or KiswahiH or both, as the case may be.
(2) The proceedings, judgment, ruling, decision, or order or decree shall be written in either ianguage and may be transiated to the other language by transiators sworn or affirmed under ruie 19 of these Rules as may be necessary. '
Tafsiri ya kifungu hicho inaweza ikawa au ikakaribiana na kusema kwamba;
'4(1)Lugha za kutumia mahakamani zitakuwa mbiii, ama Kiingereza au Kiswahili au zote mbiii, kwa kadiri itakavyokuwa.
(2) Mwenendo wa shauri, hukumu, uamuzi mdogo, uamuzi au amri au tuzo itaandikwa kwenye iugha mojawapo kati ya hizo na yaweza kutafsiriwa katika iugha nyingine kwa kumtumia mkaiimani aiiyeapishwa chini ya kanuni ya 19 ya kanuni hizi kadiri itakavyoiazimu. '
Ni katika muktadha huo hukumu hii ni ya Kiswahili ila kama nilivyosema hapo juu, itakapobidi sana ndipo Kiingereza kitatumika. Sasa niende katika maombi yenyewe yaliyo mbele ya mahakama hii.
Katika maombi haya, North Mara Gold Mine Ltd wanaomba mahakama hii iufanyie marejeo uamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Tume) katika mgogoro wa kazi namba CMA/MUS/334/2019 ambapo tume ilitoa tuzo ya jumla ya shilingi 74, 510, 509. 99 kwa mjibu maombi kwa sababu iliona kwamba uamuzi wa kumuachisha kazi ulikuwa siyo wa haki. Malalamiko ya muombaji mbele ya Tume yalikuwa ni kwamba mjibu maombi alijihusisha ni vitendo vya kihalifu; vitendo hivyo vikiwa ni kujaribu kuiba (attempted theft), kula njama za kuiba (collusion to steal) na udanganyifu au kukosa uaminifu (dishonest) kinyume na vifungu vya 3. 1, 3. 2 na 3. 13 mtawalia vya Acacia Disciplinary Procedure (ADP). Kwa mujibu wa muombaji, makosa hayo yalihusisha uhamishaji wa mafuta ya diseli kutoka katika mtambo aina ya excavator 14 (Ex. 14) na kuyahamishia katika gari jingine la kawaida lililokuwa na namba za utambulisho LV196. Mjibu maombi alikana madai hayo, ila kwa kutumia madai hayo hayo, mbele ya kamati ya maadili ya muombaji utetezi wake ukakataliwa na hatimaye akapigwa kalamu na kuoneshwa mlango mnamo tarehe 9 Disemba 2019.
Mjibu maombi alipeleka malalamiko mbele ya Tume ambayo baada ya kuyasikiliza ndipo ikabatilisha kufukuzwa kwake kazi kwa hoja kwamba muombaji hakuweza kuthibitisha makosa ya mfanyakazi juu ya urari wa uwezekano kwamba alitenda makosa hayo. Kama ilivyodokezwa hapo awali, Tume ikaamuru pia kwamba mjibu maombi alipwe jumla ya shilingi za Tanzania 74, 510, 509. 99; kiasi hicho kikiwa ni mishahara ya miezi arobaini na nane (48) sawa na shilingi 70, 127, 538. 72, mshahara wa mwezi mmoja badala ya notisi sawa na shilingi 1, 460, 990. 39 na kiinua mgongo sawa na shilingi 2, 921, 980. 88. Hizi amri ndizo zilizomghadhabisha muombaji akaamua kuwasilisha maombi haya ya marejeo mbele ya mahakama hii.
Sababu za muombaji za kupinga uamuzi wa Tume zipo katika aya ya 17 ya kiapo cha Peter Shemkai kilichowasilishwa kuunga mkono maombi. Hoja au sababu hizo ni; kwanza, kwamba Tume ilikosea kisheria kwa kuamua kwamba muombaji hakuwa na sababu za haki za kumfuta kazi mjibu maombi, piii kwamba tume katika uamuzi wake ilitumia vigezo visivyohusika na mgogoro, tatu/kwamba tume katika uamuzi wake ilipuuza ushahidi ulioletwa kuthibitisha kwamba sababu za kumfukuza kazi mjibu maombi zilikuwa za haki na mwisho kwamba tume kwa kumtuza mjibu maombi kiasi cha shilingi 74, 510, 509. 99 ilikosea kwa sababu fedha hizo ni nyingi kupita kiasi.
Hoja za kuunga mkono maombi haya kwa niaba ya muombaji ziliwasilishwa kwa njia ya maandishi na ndugu Joseph Nyerembe wakili wa mahakama hii. Katika kuelezea hoja ya kwanza, wakili alieleza kwa kirefu kwamba ushahidi wa muombaji kutoka kwa shahidi namba 1, Zirk Loubser, namba 2 Jaffari Mfinanga na namba 3 Enock Alex Nguka kwenye kurasa za 4 na 5 za hoja zake, ulithibitisha kwamba mjibu maombi alikuwa na hatia na hivyo ilikuwa haki kumfukuza kazi. Kama ilivyotegemewa, mwitikio au majibu ya ndugu Ernest Mhagama pia wakili, kwa niaba ya mjibu maombi, ilikuwa ni kukanusha vikali hoja za wakili mwenzake na kuunga mkono uamuzi na hoja za Tume.
Tofauti hii ya mitazamo, maoni na misimamo ya mawakili inayokinzana ndiyo hasa kiini kikuu ambacho mahakama hii itakizingatia na kushughulika nacho ili kutoa uamuzi. Katika kufanya hivyo mahakama itatumia hasa ushahidi wa mashahidi wa muombaji wanaotajwa kushuhudia makosa hayo bila kusahau nyaraka zilizowasilishwa mahakamani kusajili maombi haya, majibu yaliyowasilishwa na mjibu maombi pamoja na hoja za maandishi za mawakili. Chanzo kingine bila shaka itakawa ni kumbukumbu za tume.
Kama ilivyoelezwa awali, kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mbele ya kamati ya maadili mfanyakazi alishitakiwa kwa kwa makosa yafuatayo kwa kuyanukuu yalivyoandikwa;
'COUNT ONE
Attempted theft of Company property contrary to offence category 3 sub category 3. 1 of the BARRICK Discipiinary Code.
PARTICULARS OF BREACH
That on 15th September 2019, at around 09:53 Hrs while on duty at the Rama Tower 03, driving LV 196, you attempted to steal Fuel from Excavator 14, while knowing that doing so amount (sic) to the vioiation of the aforementioned rule.
COUNT TWO
Collusion to steal company property contrary to offence category 3 sub category 3. 2 of the BARRICK Disciplinary Code.
PARTICULARS OF BREACH
That on 15th September 2019, at around 09: 53 Hrs while on duty at the Rama Tower 03, while driving LV 196 you colluded with Alexander Andrew Mtenga to steal Fuel from Excavator 14, while knowing that doing so amount (sic) to the vioiation of the aforementioned rule.
COUNT THREE
Committing an act amount (sic) to dishonest in performance of duty contrary to offence category 3 sub category 3. 13 of the BARRICK Disciplinary Code.
PARTICULARS OF BREACH
That on 15th September 2019, at around 09:53 Hrs while on duty at the Rama
Tower 03, whiie driving LV 196, with an intention to act dishonestiy, you drained fuel out of Excavater 14 and refiii LV 196 while knowing that doing so amount (sic) to the vioiation of the aforementioned rule. '
Hayo ndiyo makosa ambayo muombaji alitakiwa kuyathibitisha juu ya urari wa uwezekano kwamba mjinu maombi aliyatenda na hoja ya Ndugu Nyerembe ikawa ni kwamba kwa ushahidi wa ndugu Zirk Loubser makosa yalithibitika.
Kwanza Kanuni ya 9 (3) ya the Employment and Labour Relations (Code of Good Practice) Rules 2007, GN 42 of 2007 inasema kwamba;
'The burden of proof lies on the employer but it is sufficient for the employer to prove the reason on the balance of probabilities. '
Kwa Kiswahili tunaweza kutafsiri kifungu hicho kama ifuatavyo;
'Jukumu ia kuthibitisha uhaiali wa kumfukuza kazi mfanyakazi ni ia mwajiri, iia inatosha kwa mwajiri kuthibitisha uhaiaii huo kwa kiwango cha urari wa uwezekano. '
Nitaanza na hilo; kama mwajiri alithibitisha uhalali wa kumfukuza mfanyakazi kwa kiwango hicho. Kwa mujibu wa ndugu Nyerembe, ushahidi wa upande wa utetezi mbele ya tume ulithibitisha uhalali huo.
Kwanza nitashughulika na kiwango cha kuaminika cha shahidi wa utetezi, ndugu Zirk Loubser, kwa sababu ndiye shahidi pekee aliyeona kilichotokea kwanye eneo la tukio wengine walikuja baadae. Kwa mujibu wa kumbukumbu za kamati ya nidhamu hususan waraka unaoitwa
'Statement of Complainant' Zirk Loubser alisema hivi;
'Mimi na Frank tuiikuwa view point at Rama pit Ex 14 iiikuwa kuiia kwetu na service tank iiikuwa kando, wakati tunarudi nikaona kwenye Ex 14 gari ndogo ilikuwa imepaki na wamechukua pipe wakivuta mafuta. Nikaenda kwenye Ex 14 kuona kinachoendeiea, LV196 iiikuwa impeki chini ya Ex 14 na kuiikuwa na pipe ikivuta mafuta na gari ilikuwa ipo on. '
Kwa ushahidi huu, kinachoonekana ni kwamba ndugu Zirk Loubser aliona mafuta yakinyonywa kutoka kwenye Ex 14 na kuingizwa kwenye gari LV196. Hata hivyo ushahidi wake mbele ya tume, haukuwa huu hata kidogo; mbele ya tume ukurasa 8 (ulioandikwa kwa mkono, sababu kumbukumbu hazijachapwa) shahidi huyu alisema hivi;
Excavater 14 was decommissioned since June (was not working). The action of seing someone there while the machine was not working was something diff (sic). We decided to go there, we went there and we saw LV196. Frank was there and I find (sic) the LV was idol (sic) no ongoing was not there (sic). No body was in the LV. I picked up the pipe there was diesel fuel running out. Frank notified that the fuel tank was full. I also confirmed that the fuel was full. LV196 I noticed both fuel tanks were ciosed. There were fuel drops on the side of LV196 (on the ground). Frank called security controi and I proceeded to Excavator. I noted there is electric fence compound and I find (find) two persons Gerald and Alex. Gerald was inside the compound working... Alex was standing across the door, I greeted them and asked what they were doing and they stayed quiet.... '
Mahakama hii ikiulinganisha ushahidi huu wa ndugu Zirk Loubser alioutoa mbele ya tume, na malalamiko aliyoyatoa mbele ya kamati ya nidhamu iliyomfukuza kazi mjibu maombi haioni ulinganifu. Mbele ya kamati ya maadili anasema aliona kitendo cha kuvuta mafuta ila mbele ya tume anasema aliona bomba likiwa na mafuta ya diseli. Kama shahidi huyu angalikuwa anaaminika, asingalikuwa na ndimi mbili; angalikuwa na hadithi ile ile, iwe mbele ya kamati au mbele ya tume. Kwa tofauti hizi za ushahidi wa mtu huyo huyo, ushahidi wa ndugu Zirk Loubser ni wa kutilia mashaka sana na hauaminiki.
Ushahidi wa ndugu Jafarry Mfinanga na ndugu Enock Alex Nguka ni kwamba gari LV196, haikutakiwa kuwa imejaa mafuta tarehe 15 Septemba 2019 sababu ilikwishatembea kilometa, 488 tangu kuwekewa mafuta siku 7 zilizotangulia. Huu ushahidi unaingiwa na kasoro kutokana na waraka wa Mwenyekiti wa Kamati ya nidhamu wenye kichwa cha habari 'Alexander Mtengwa and Gerald Nzumbi Attempted Theft Case Hearing by Dr. Nichoias P. Mboya (Hearing Chairma) 'ambao katika pointi namba 11 mwenyekiti anaandika hivi;
'11. The distance covered by LV196 since the last refuei was 488KM and wouid be expected to remained (sic) with not more than 110 iiters in both tanks, calculated under Toyota Manufacturers fuel usage specifications. This means that one tank wouid been (sic) expected to be full and the other one wouid be expected to be less (or both couid be less)'.
Hii ina maana gani? Ina maana kwamba, hata bila kuongeza mafuta yoyote, kama gari lilijazwa mafuta matanki yote mawili tarehe 08. 09. 2019, inawezekana kwamba tarehe 15. 09. 2019 matanki yote mawili yakawa hayakujaa au mojawapo likawa limejaa na jingine likawa halikujaa. Kama kulikuwa na uwezekano kwamba tanki mojawapo linaweza kuwa limejaa mafuta tarehe 15. 09. 2019 kuna uwezekano pia kwamba tanki lilokaguliwa huenda ndilo lililokuwa limejaa kwa mujibu wa hoja hiyo ya mwenyekiti. Kwa pointi namba 11 ya mwenyekiti ushahidi wa ndugu Jafarry Mfinanga na ndugu Enock Alex Nguka unatiwa kasoro inayouondolea nguvu.
Pamoja na udhaifu wa ushahidi wa upande wa mwajiri, kwa namna nilivyomuelewa ndugu Nyerembe, vyombo vyote viwili yaani Ex 14 na LV196, vilikuwa ni mali ya muombaji. Kama hivyo ndivyo, na hata tukasema kwamba mafuta yalitolewa kwenye mtambo Ex 14 na kuwekwa kwenye LV196, na kweli tukasema yaliwekwa na mjibu maombi, hilo tendo kwa viwango vyovyote vile, linawezaje kupelekwa kwenye tafsiri za kujaribu kuiba, kuia njama za kuiba, na udanganyifu au kukosa uaminifu?. Kwa upande wa ndugu Nyerembe na muombaji wanaweza kuona kuwa hayo ni makosa ya kijinai, ila kwa mahakama, kila nikijaribisha kupeleka hilo jambo kwenye hayo makosa inashindikana. Hiyo ni kama mtu kutoa fedha kwenye mfuko wake mmoja akaziweka kwenye mfuko mwingine wa nguo yake hiyo hiyo aliyoivaa. Nikijiuliza ni vipi mjibu maombi ananufaika na mafuta anayoyaweka kwenye gari la mwajiri wake sipati jibu la haraka ambalo ni la kimantiki achilia mbali la kisheria.
Katika kujaribu kuiba ni pale mtu anachukua kitu kisicho chake akiwa na dhamira kwamba mwisho kiwe chake, lakini kwa namna moja au nyingine uchukuaji huo usikamilike. Kwenye hili lililo mbele yetu ni kitu gani kinaonyesha kwamba mafuta yaliyotolewa kwenye katapila la mwajiri yakawekwa kwenye gari jinigine la mwajiri yalikuwa yanataka kuibiwa na dereva? Ni maoni ya mahakama hii kwamba ni tofauti kama dereva huyo angekutwa na vyombo vyake binafsi amevijaza mafuta kutoka kwenye Ex 14 au kama angekutwa ananyonya mafuta kutoka kwenye Ex 14 na kuyaweka kwenye gari lake binafsi, hapo unaweza kuongelea habari ya kuiba au kujaribu kuiba. Ila katika mazingira haya ambapo mwajiri anasema mfanyakazi wake mwenyewe alitoa mafuta kwenye mtambo mmoja ambao haufanyi kazi akayaweka kwenye gari linalofanya kazi, haieleweki hata kidogo kujaribu kuiba kunaingiaje kwenye maelezo, hata kama mjibu maombi angekamatwa akifanya hilo jambo. Ninalosema hapa ni kwamba, haieleweki ni kwa nini kosa halikuwa kutoa mafuta kwenye mtambo na kuyaweka kwenye gari badala yake mwajiri akakurupukia kusema kwamba kulikuwa na jaribio la wizi. Kwa maneno mepesi zaidi ni hivi, kama kuna kosa ambalo nalo sikuona kama kuna shahidi aliyelithibitisha, lingekuwa ni kutoa mafuta kwenye mtambo mmoja wa muombaji na kuyahamishia kwenye gari la mtu huyo huyo.
Mwisho kuhusu hili la jaribio la kuiba, kama muombaji alimkuta mjibu maombi anatoa mafuta kwenye mtambo mmoja na kuyaweka kwenye gari la kampuni hiyo hiyo, muombaji alitakiwa kwenda kwenye kanuni zake Acacia Disciplinary Procedure na kama angekuta kufanya hivyo ni kosa angechukua hatua kulingana na kanuni ambavyo zingekuwa zinasema lakini siyo kulazimishia mambo yasiyokuwepo kama alivyofanya kwenye kesi hii. Kwa ufupi, tume ilikuwa sahihi ilipoamua kwa kusema kuwa hakukuwa na uthibitisho wowote kuonyesha kwamba kulikuwa na jaribio la wizi. Sasa nihamie kwenye kosa la kula njama.
Kwanza ili kula njama ni lazima kuwe na watu zaidi ya mmoja, ila pia kwenye hii kesi ilikuwa ni kula njama ya kufanya nini. Vyovyote vile ilikuwa ni kula njama ya kuiba. Ila nimesema hapo juu achilia mbali kuiba, hata kujaribisha kuiba hakukuthibitishwa kwa hiyo mahakama hii haioni na vipi tume ilitakiwa ikubaliane na jambo ambalo halikuwepo kabisa maana kula njama ni kufanya njama za kutenda uhalifu jambo ambalo halikuwepo. Mwisho ni udanganyifu au kukosa uaminifu. Hili jambo kwa viwango vyovyote vile, halikuthibitishwa. Kunaweza kukawa na udanganyifu kukionyeshwa, kwamba mjibu maombi alitaka kwa namna moja au nyingine kunufaika na jambo hilo kwa kumtia hasara muombaji. Yaani ilitakiwa ioneshwe kwamba baada ya kuweka yale mafuta kwenye LV196 basi gari lilikuwa linatumiwa na mjibu maombi kwa ajili ya kazi zake binafsi, kinyume na hapo, hata ukikaa mwaka mzima unatafuta udanganyifu hautaupata.
Ni uamuzi wa mahakama hii, kwamba tume ilikuwa sahihi kwa kuamua kwamba muombaji hakuthibitisha kwamba alikuwa na sababu ya haki kumfukuza kazi mjibu maombi kama inavyotakiwa na kifungu cha 37(2) cha the Employment and Labour Relations Act, no 6 of 2004.
Kulikuwa na hoja tatu, na tumemaliza ya kwanza; bado ya pili ya tatu na ya nne. Kwa kujikumbusha tu, ya pili ilikuwa ni kwamba tume katika uamuzi wake ilitumia vigezo visivyohusika katika mgogoro, tatu kwamba tume ilipuuza ushahidi ulioletwa kuthibitisha kwamba sababu za kumfukuza kazi mjibu maombi zilikuwa za haki na nne kwamba tume kwa kumtuza mjibu maombi shilingi 74, 510, 509. 99 ilikosea kwa sababu fedha hizo ni nyingi kupita kiasi.
Kuhusu hoja ya pili, hata kama tume ingetumia vigezo gani, hakuna namna ambavyo sababu za kumfukuza kazi mjibu maombi zingeweza kuwa za haki, kulingana na mjadala katika kushughulika na hoja ya kwanza. Hoja ya tatu nayo ni kama ile ya kwanza. Ushahidi wote ulioletwa ni wa kuonyesha kitu hicho hicho, matone ya mafuta ya gari, bomba pamoja na gari LV196 likiwa limejaa mafuta, huenda, yaliyotoka kwenye mtambo Ex 14. Kwenye hoja za maandishi sikuona ushahidi unaosemekana kwamba tume haikuutilia maanani. Kwa hiyo hii mahakama haioni jipya lolote katika lalamiko la 3 la muombaji.
Mwisho ni kiasi cha tuzo kilichotolewa cha mishahara ya miezi 48. Wakili Nyerembe anasema kwamba tume ilikosea kwa sababu kanuni ya 32(5) ya the Labour Institutions (Mediation and Arbitration) Rules 2007 TS namba 64 la 2007 inamtaka Muamuzi kumtuza fidia ya chini kabisa iwezekanavyo mfanyakazi. Ndugu wakili akaiomba mahakama kutumia pia kifungu kifungu cha 40 cha Employment and Labour Relations Act namba 6 ya 2004, ili mfanyakazi alipwe kiasi kisichozidi mishahara ya miezi 12 kadiri ya kifungu hicho. Kwanza kanuni ya 32(5) ya the Labour Institutions (Mediation and Arbitration) Rules 2007 TS namba 64 la 2007 haina uhusiano kabisa na mambo ya mfanyakazi na mwajiri kulipana fidia baada ya mgogoro kwisha mbele ya tume au mahakamani. Kanuni inahusu uandishi wa kumbukumbu katika migogoro ya kazi. Hii itoshe kuonesha aina na thamani ya msaada wakili alioutoa kwa mahakama yeye kama afisa wa mahakama anayetakiwa kuisaidia kufikia maamuzi ya haki. Sasa nije kwenye kifungu cha 40(l)(c) cha sheria namba 6 ya 2004 ambacho wakili alisema kinaitaka mahakama au tume kuamuru kiasi cha fidia kisichopindukia au kisichozidi mishahara ya miezi 12. Kifungu hicho kinaelekeza hivi;
'40(1) If the Arbitrator or the Labour Court finds a termination is unfair the arbitrator or the Court may order the employer: -
(c) to pay compensation to the empioyee of not less than twelve months' remuneration. '
Hicho kifungu cha sheria kwa Kiswahili kinaweza kutafsiriwa kuwa na maana ifuatayo;
'40(1) Kama Muamuzi au Mahakama ya Kazi ikijiridhisha kwamba kufukuzwa kazi kwa mfanyakazi hakukuwa kwa haki, Muamuzi au Mahakama hiyo yaweza kumuamuru mwajiri: -
(c) kumiipa mfanyakazi kiasi kisichopungua maiipo ya miezi kumi na miwiii.
Hapa pia hoja ya wakili kwamba fidia haitakiwi kuzidi mishahara ya miezi 12 endapo mwajiri amemwachisha kazi mtumishi isivyo halali, haieleweki, siyo tu kwa mwanasheria lakini kwa mtu yeyoye baki kwa sababu kifungu cha sheria kiko wazi sana. Kwa hoja hiyo pamoja na nyingine ndogo ndogo kuhusu swala la fidia nazitupilia mbali, halina uzito wowote kisheria. Labda niseme kwamba jambo lililoniongoza ni; je muamuzi alikuwa na mamlaka ya kutoa fidia ya miezi 48 au hakuwa nayo. Kwa kusoma kifungu namba 40(l)(c) cha sheria namba 6 ya 2004 nilichokinukuu hapo juu muamuzi alikuwa na mamlaka kuamuru kulipwa kwa fidia kadiri alivyoamua.
Katika mgogoro ulipelekwa mbele ya tume muamuzi hakuona sababu yoyote ya kisheria ambayo ingemfanya muombaji kumfukuza kazi mjibu maombi. Mahakama hii nayo pia, haioni sababu zozote za kisheria za kutofautiana na tume, achilia mbali kutengua uamuzi wake. Kwa kuzingatia sababu zilizojadiliwa katika hukumu hii, maombi haya ya marejeo yemetupiliwa mbali na tuzo ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi katika mgogoro wa kazi namba CMA/MUS/334/2019 imethibitishwa kuwa halali na itatekelezwa kama ilivyotolewa mnamo Julai 30, 2020.
Mwisho kabisa upande usioridhika na hukumu hii una haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
IMETOLEWA hapa MUSOMA Tanzania, leo tarehe 22 Januari 2021
Z. N. Galeba
JUDGE
22. 01. 2021