HOTUBA YA PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA, JAJI MKUU WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MAJENGO YA VITUO SITA JUMUISHI VYA UTOAJI HAKI VYA DODOMA, MWANZA, ARUSHA, MOROGORO, TEMEKE NA KINONDONI TAREHE 06 OKTOBA, 2021 – JIJINI DODOMA
Download:
HOTUBA YA PROF. IBRAHIM HAMIS JUMA, JAJI MKUU WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MAJENGO YA VITUO SITA JUMUISHI VYA UTOAJI HAKI VYA DODOMA, MWANZA, ARUSHA, MOROGORO, TEMEKE NA KINONDONI TAREHE 06 OKTOBA, 2021 – JIJINI DODOMA
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu;
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama;
Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani Mliopo;
Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Mbunge);
Mhe. John Samuel Mgetta, Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
Mhe. Mustapher Siyani, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma;
Wahe. Majaji wa Wafawidhi Vituo Jumuishi-Arusha, Mwanza, Morogoro na Temeke;
Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu mliopo;
Mhe. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria;
Wahe. Mawaziri wengine wote na Manaibu Waziri mliopo;
Mhe. Anthony John Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Mhe. Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama;
Mhe. Wilbert Chuma, Msajili Mkuu wa Mahakama;
Wahe. Makamishna, Tume ya Utumishi wa Mahakama;
Bi. Enziel Mtei, Naibu Katibu Tume ya Utumishi ya Mahakama;
Wahe. Wasajili, Watendaji na Manaibu Wasajili mliopo
Wahe. Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu mliopo
2 | P a g e
Wahe. Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati Mbalimbali za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Sylvester Mwakitalu, Mkurugenzi wa Mashtaka;
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
Bi. Deborah Isser (Kiongozi wa Kikundi Kazi cha Mradi wa Benki ya Dunia) akisaidiwa na Bw. Waleed Malik pamoja na maafisa wengine wa Benki ya Dunia; Ambao wako pamoja na sisi kwa njia ya VIDEO.
Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali vya Mahakama ya Tanzania; NA WATUMISHI WOTE WA MAHAKAMA
Mahakimu, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea mliopo;
Viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa na Madhehebu ya dini mliopo;
Wana Habari wote mliopo;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
NAWASALIMIA KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Mheshimiwa Rais, Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, muweza wa yote kwa kutujalia ruzuku ya afya njema na kutukutanisha salama hapa jijini Dodoma, Makao Makuu ya Nchi yetu. Kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania na kwa niaba yangu binafsi nakushukuru sana, Mheshimiwa Rais, kwa kukubali mwaliko wangu wa kuja kutuzindulia majengo ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki: DODOMA, MWANZA, ARUSHA, MOROGORO, KINONDONI na TEMEKE.
3 | P a g e
Mheshimiwa Rais, kuwepo kwako hapa leo pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali na Kiongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kielelezo tosha kuwa mihimili yote mitatu ya Dola inashirikiana kwa ukaribu katika ujenzi wa Tanzania moja inayozingatia misingi ya UHURU, HAKI, UDUGU, AMANI na inayolenga kudumisha ustawi wa wananchi wa Tanzania. Mheshimiwa Rais NAKUKARIBISHA SANA!
Mheshimiwa Rais, kwa miaka sita iliyopita, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikitekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ulioambatana na Programu ya Maboresho. Falsafa inayosukuma maboresho ya mahakama ya Tanzania imejengwa katika dhana iitwayo CITIZEN-CENTRIC JUSTICE SERVIVE DELIVERY—yaani huduma ya utoaji haki inayowalenga wananchi. Dhana hii imebebwa na uelewa kwamba, huduma za utoaji haki ni huduma za lazima na muhimu kwa umma; na kwamba, maboresho makubwa yanayoendelea ndani ya Mahakama, ni sehemu ya mikakati ya maboresho ya nchi yetu yanayolenga kuyafikia Malengo Makuu Matano yanayosisitizwa na DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2025 ambayo Serikali yako na Bunge imeazimia kuyafikia. Tumekumbushwa mara kadhaa kuwa, Dira ya Maendeleo 2025 ni mwongozo au mwelekeo wa Tanzania kama TAIFA linavyotaka kuwa itakapofika mwaka 2025. Majengo haya Jumuishi ndio picha ya Mahakama ya Tanzania inavyotakiwa kuwa ifikapo 2025. Mchango wa Mhimili wa Mhimili wa Mahakama kufanikisha DIRA YA MAENDELEO unaonekana wazi wazi katika Lengo Kuu la Pili la “Kuwepo kwa mazingira ya amani, usalama na umoja”; na Lengo Kuu la Tatu la “kujenga
4 | P a g e
utawala bora.” Mahakama ya Tanzania inaamini kuwa, kwa kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi, Mahakama sio tu inachangia uwepo wa amani, utulivu na utawala bora hapa nchini Tanzania; bali pia, Mahakama inachangia kuiwezesha Tanzania kufikia Lengo Kuu la Tano la DIRA YA MAENDELEO, la “kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.” Maboresho ya Mahakama yanatambua kuwa, migogoro inapowasilishwa Mahakamani, basi ikamilike kwa haraka ili wananchi, wafanya biashara na wawekezaji, watumie muda wao mwingi zaidi na rasilimali zao, kuzalisha mali na kutoa huduma. Tasnifu kuu hapa (the main thesis) ni kwamba, maboresho ya Mahakama ni uwekezaji unaofanywa na Tanzania katika safari ya kuyafikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Mheshimiwa Rais, uzinduzi wa vituo sita jumuishi ulioufanya leo, ni uwekezaji mkubwa wenye multiplier effect katika kufikia malengo makuu matano yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Tukio la leo ni hatua muhimu katika safari ndefu ya Mahakama kusogeza huduma za utoaji haki.
Mheshimiwa Rais, leo ni siku ambayo dhana ya wajibu wa msingi wa Serikali, KUUWEZESHA Mhimili wa Mahakama katika kufanya kazi ya utoaji haki linajitokeza wazi wazi. Vituo Jumuishi hivi ni vielelezo kuwa mzigo wa Mahakama kupata miundombinu ya majengo ni mzigo unaobebwa na uwezeshaji wa Serikali unayoiongoza pamoja na ridhaa ya Bunge. Mzigo huu umejionyesha kwa utayari ulioonyeshwa na Serikali yako kutafuta
5 | P a g e
Mkopo wa Benki ya Dunia kuiwezesha Mahakama kupata majengo ya kisasa na kusogeza ngazi za utoaji haki karibu zaidi na wananchi. Binafsi, nitakosa shukrani kama sitatambua mchango mkubwa wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman na Balozi Hussein Kattanga ambao waliasisi wazo la Mahakama kuwa na Mpango Mkakati, na potential ya huo Mpango Mkakati ulizaa programu ya maboresho—Judiciary-led reforms.
Vituo hivi sita Jumuishi pia vimebeba dhana muhimu ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kwa faida ya uboreshaji wa utoaji na upatikanaji wa haki hapa Tanzania. Andiko la mradi uliofanywa na Benki ya Dunia kuhusu mradi uliozaa vituo hivi (Tanzania Citizen-Centric Judicial Modernisation and Justice Service Delivery Project), imefafanua madhumuni ya ujenzi wa vituo hivi jumuishi:
“Majengo haya jumuishi ni vielelezo vya maboresho ya huduma za utoaji haki. Moja ya maeneo ya maboresho hayo ni kusogeza huduma za kimahakama karibu na wananchi ili kuwezesha huduma hizo kupatikana katika eneo moja na kwa urahisi. Hii ni pamoja na kuwa na huduma katika eneo moja linalojumuisha ngazi tofauti za mahakama na wadau ambao wanashirikiana na Mahakama katika kutoa huduma za haki —Integrated Justice Centre).”
6 | P a g e
Mheshimiwa Rais, kipekee, naomba kutambua maafisa wa Benki ya Dunia ambao wanaunda Kikundi Kazi (TASK FORCE) kinachoiwakilisha Benki ya Dunia katika usimamizi wa Maboresho ya Mahakama: Bi. Deborah Isser (Team Task Leader); Bw. Waleed Malik (Co-Team Task Leader); Bi. Clara Maghani (World Bank Specialist); na Bw. Benjamin Mtesingwa (World Bank Specialist).
Mheshimiwa Rais, muasisi wa dhana ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ni Bwana Waleed Malik, Mtaalamu Mwandamizi wa Menejimenti ya Sekta ya Umma katika Benki ya Dunia. Dhana hii inatekelezwa nchini Ufaransa katika jiji la Paris ambapo katika jengo moja la Mahakama linahuduma zote za wadau wa huduma za haki. Hali kadhalika nchini Guatemala iliyoko Amerika ya Kati, ambao mfumo wao una ngazi zote nne za Mahakama kwenye jengo moja, ukijumuisha ofisi za wadau muhimu katika mnyororo wa utoaji haki. Aidha, Mahakama hizi pamoja na kutumia Teknolojia zaidi pia huduma zinatolewa masaa 24.
Mheshimiwa Rais, kufanikisha uanzishaji wa vituo jumuishi hapa nchini kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kutoa huduma jumuishi za utoaji haki chini ya paa moja (Justice services under one roof). Vituo hivi jumuishi pia vitaiwezesha Tanzania kuongezewa alama za upimwaji wa huduma za utoaji haki katika mizani ya wananchi kuridhishwa na ubora wa huduma zetu. Vituo hivi pia vitasaidia upimwaji wa Mahakama ya Tanzania katika vipimo vya kimataifa, kwa mfano
7 | P a g e
Vipimo vya Urahisi wa Kufanya Biashara (Doing Business Report), utafiti unaopima mitazamo ya jamii katika maswala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo utawala wa sheria na utoaji haki (AFROBAROMETER).
Aidha, baada ya Mheshimiwa Rais kuzindua hivi vituo leo hii, Tanzania itakuwa ni eneo la mfano na la kujifunza kwa nchi nyingine. Nawasihi watumishi watakaotoa huduma katika vituo hivi, jitayarisheni kuwapokea wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania, watakaofika kujifunza maboresho ya huduma za utoaji haki ndani ya vituo hivi. Kwa muda wa miaka mitano ya Maboresho (2016/17-2019/21), Mahakama ya Tanzania imekuwa ikipokea wageni wanaokuja kujifunza maboresho yanayoendelea hapa nchini. Mfano, Mhe. Jaji Mkuu wa Ethiopia (MEAZA ASHENAFI), Jaji Mkuu wa Guatemala, viongozi kutoka Mahakama ya Uganda wamewahi kufanya ziara za kujifunza na kubadilishana uzoefu katika maboresho ya mahakama. Wageni wengi watafika kutaka kujua namna haki inavyotolewa katika vituo hivi sita jumuishi. Leo hii uki-google “integrated justice centres,” utakuta Habari za Mahakama ya Tanzania kuanza ujenzi wa vituo jumuishi vya utoaji haki. Baada ya uzinduzi wa leo, google itatangaza kuwa ujenzi wa vituo jumuishi zimezinduliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Rais, utekelezaji wa maboresho ya Mahakama, pia umetokana na ziara za kubadilishana uzoefu katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Guatemala mwaka 2017 na
8 | P a g e
Ufaransa kwa lengo la kujifunza, pamoja na mambo mengine, namna bora ya kuongeza upatikanaji wa huduma za utoaji haki kupitia dhana hii ya vituo jumuishi vya utoaji haki na Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ambapo baadhi ya maafisa wa Mahakama walifanya ziara hizo. Nawaomba watumishi wote watakaopata bahati ya kuhudumia katika vituo hivi, tuendelee kujifunza kutoka ndani na nje ya Tanzania. Tuwe wepesi kupokea ushauri.
Mheshimiwa Rais, Andiko la mradi wa maboresho, Pamoja na maandiko mbali mbali ya Mahakama ya Tanzania yametaja faida nyingi ambazo zitapatikana baada ya uzinduzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki. Naamini kuwa ni matarajio yako, na ya watanzania wote kuwa hizi faida zitatoka katika maandiko na kupatikana kiuhalisia:
1. Majengo haya jumuishi yamebeba faida ya kuwapunguzia wananchi na wadaawa gharama na muda wanaotumia katika kufuatilia huduma za haki ambazo zinatolewa na wadau tofauti katika sehemu tofauti kwa kuwa utoaji wa huduma jumuishi unarahisisha huduma hizo kupatikana katika eneo moja la jengo moja la Mahakama lenye wadau wote muhimu katika usikilizaji wa shauri.
2. Vituo Jumuishi vitasaidia katika Usimamizi na ufuatiliaji wa utoaji wa huduma za kimahakama kuweza kufanyika kwa haraka na katika utaratibu wa kila siku au pale tatizo linapojitokeza tofauti na hali ya sasa ambapo ushughulikiaji
9 | P a g e
wa jambo au tatizo linapojitokeza huchukua muda au kusubiri mpaka ukaguzi wa robo mwaka kufanyika.
3. Vituo hivi vitachangia katika kupungua kwa gharama za uendeshaji wa shughuli za kiutawala na kimahakama kwa kuwa rasilimali inatumika katika eneo moja au jengo moja badala ya majengo matatu ya mahakama ya ngazi tofauti, na ofisi za wadau zote pamoja na ngazi zote za mahakama watafaidika na unafuu wa gharama kama za maji, umeme, ulinzi, usafi na hata usafiri wa watumishi.
4. Vituo jumuishi vitakuwa sehemu ya Matumizi sahihi ya rasilimali mali watu kwa kuwa huduma zote zinapopatikana katika eneo moja katika utaratibu mzuri zitatolewa na watumishi wachache, tofauti na idadi ya watumishi inayotumika kama ngazi za mahakama zinakuwa katika maeneo na sehemu tofauti.
5. Matumizi ya TEHAMA katika vituo hivi yatapunguza gharama za uendeshaji kupitia mifumo itakayotumika ambayo itapunguza matumizi ya wino, karatasi, majalada, kalamu “stationaries” makabati ya kutunzia nyaraka n.k. ambavyo vimekuwa na bajeti kubwa katika uendeshaji.
6. Vituo hivi Jumuishi vitakuwa vitovu vya matumizi ya teknolijia kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi. Kwa kutambua kuwa, pamoja na kuwa na huduma za ngazi zote za Mahakama ndani ya jengo moja,
10 | P a g e
bado wananchi wengi watakuwa bado wako mbali na majengo haya. Kwa hiyo, mifumo ya teknolojia na vifaa vya TEHAMA vitawasogeza wananchi walio mbali na majengo haya kupata huduma kama nakala za hukumu `na taarifa za mashauri yao kupitia taarifa fupi za SMS, video conference, TOVUTI, JSDS2, na TANZLII.
7. Mifumo ya Tehama itayotumika itapunguza idadi ya watumishi kwa kuwa mifumo hii itafanya kazi ambazo hapo awali ilihitaji uwepo wa idadi kubwa ya watumishi.
8. Matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa mashauri, utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa taarifa na ushughulikiaji wa kero za wadaawa, utaongeza ufanisi, uwajibikaji na uwazi katika upatikaji wa huduma za haki na kuongeza Imani ya wananchi kwa Mahakama na kwa taifa kwa ujumla.
MAGARI YA MAHAKAMA ZINAZOTEMBEA (MOBILE COURTS) NA VITUO JUMUISHI
Mheshimiwa Rais, kwa kusisitiza kuwa hata baada ya kujengwa kwa vituo hivi jumuishi bado kutakuwa na wananchi ambao watabaki mbali, kwa kutembea mwendo mrefu kufuata huduma za Mahakama; baadhi ya vituo Jumuishi vitakuwa na magari ya Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ambazo zitakuwa ni sehemu ya vituo jumuishi katika kufikisha huduma hizi karibu na mwananchi kama inavyofanyika katika mikoa ya Dar es salaam
11 | P a g e
na Mwanza. Magari haya yatakuwa na vifaa vyote vya TEHAMA na yatakuwa yakiwasiliana na Kituo Jumuishi kwa kutumia mifumo ya Kielektroniki. Hivyo basi, kupitia MOBILE COURTS, vituo hivi jumuishi vitatembea na kuwafuata wananchi na kuwaunganisha na huduma za vituo jumuishi.
Tunatarajia Serikali itakapokamilisha makubaliano na Benki ya Dunia ya mkopo wa awamu ya pili ya mradi wa maboresho ya huduma za utoaji haki, magari haya yatanunuliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi mapema mwaka 2023.
KWA NINI KITUO JUMUISHI JIJINI DODOMA?
Mheshimiwa Rais, nyuma ya kila kituo jumuishi ulichokizindua leo hii, kuna majadiliano marefu baina ya Serikali ya Tanzania, Mahakama ya Tanzania na Benki Kuu ya Dunia. Kila kituo Jumuishi kina majibu ya SWALI kwa nini kilijengwa hapo kilipojengwa. Kwa mfano, Kituo Jumuishi Dodoma ni kwa sababu Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi. Kuhamia kwa shughuli za kiserikali na Bunge Jijini Dodoma imeongeza idadi ya watu. Shughuli za kibiashara na kiuchumi zimeongeza mahitaji ya huduma za utoaji haki. Migogoro ya kijamii na ya kibiashara katika Jiji ambalo ni Makao Makuu ya nchi inahitaji Mahakama yenye miundombinu bora na ya kisasa inayokidhi vigezo vya kimataifa.
12 | P a g e
Mheshimiwa Rais, ni vigumu kuzungumzia Kituo hiki Jumuishi hapa Dodoma bila kukumbuka hali ya utoaji haki aliyoikuta Jaji Mzungu GILCHRIST ALEXANDER wakati wa utawala wa waingereza aliyefika Dodoma kwa treni mwaka 1921 ili asikilize mashauri ya Mahakama Kuu. Jaji ALEXANDER alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanganyika kati yam waka 1921 na 1925 (wenyeji ndio walimbandika jina la Jaji Mwenye Kanzu Nyekundu), alikuwa Jaji wa kwanza wa wakati wa utawala wa Waingereza Tanganyika kutumia Reli ya Kati, kuleta huduma za Mahakama Kuu hapa Dodoma. Miaka hiyo ya 1920, HAKI katika ngazi ya Mahakama Kuu, mwanzoni ilipatikana mjini Dar es Salaam tu na baadaye haki ilisogezwa katika miji iliyokuwa ikifikika kwa treni, yaani Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Dodoma, Tabora hadi Kigoma; na reli ya Tanga.
Jaji Mwenye Kanzu Nyekundu alisisitiza umuhimu wa shamra shamra (pomposity and ceremonies) ambazo majaji huonyesha wazi wazi. Alijitetea kwa kusema wananchi wa Tanganyika lazima waone utofauti wa utawala wa mwingereza Tanganyika ulioanza mwaka 1920, ni utawala mpya na unaleta utukufu wa sheria (majesty of the law):
"…..Kikao cha kwanza kabisa kufanyika Dodoma kilifanyika Bomani.
Machifu walifurika kuja kuona namna haki inavyotolewa na Jaji mzungu kutoka Uingereza. Wananchi walitembea kutoka vijiji vya mbali kutoka Dodoma na Bomani palifurika. Mavazi yao yalikuwa
13 | P a g e
yamejaa vumbi. Mavazi yaliyovaliwa yalikuwa ni mchanganyiko wa mavazi yaliyotengenezwa kutoka ngozi za ngómbe, za mbuzi, na nguo ambazo ilikuwa vigumu kwa Jaji Mwenye Kanzu Nyekundu kuweza kujua ni rangi gani kwa sababu ya uchakavu na vumbi. Nguo zilizovaliwa zilifunika sehemu chache tu za miili. Sehemu nyingi za mwili zilikuwa nyeusi zilizongára kutokana na jua kali kuchoma miili iliyokuwa ikitoka jasho.
Baadhi ya wananchi walifika hapo bomani kulipa kodi. Wengine walifika kusikiliza orodha ndefu ya mashauri ya Mahakama Kuu. Wengine walifika kuonana na viongozi wa Serikali, kwa mfano, maafisa kilimo, maafisa mifugo, wa hapo bomani. Ndani ya ukumbi wa Mahakama waliketi machifu, wajumbe na Maliwali, ambao miongoni mwao waliteuliwa kuwa Wazee wa Baraza (Assessors) kumsaidia Jaji kufikia maamuzi. Kwa muda aliokuwa Dodoma, Jaji Alexander alisikiliza kati ya kesi 20 hadi 30 nyingi zilikuwa ni za kutoka wilaya za mbali kutoka Dodoma.
Washtakiwa na mashahidi walitembea kwa miguu kwa siku kuanzia nane hadi kumi ili kufika Dodoma kwa ajili ya Mashauri ya Mahakama Kuu.
14 | P a g e
…..kesi nyingi zilizosikilizwa na Mahakama Kuu Dodoma zilikuwa za jinai, kwa mfano mauaji ya kukusudia, kujeruhi, ubakaji, unyangányi wa kutumia nguvu au silaha. Kesi nyingi zilitokana na ulevi wa pombe. Matumizi ya pombe yaliongezeka sana mara baada ya mavuno. Uhalifu pia uliongezeka wakati wa mavuno. Ilikuwa ni jambo la kawaida kuwaona wananchi wakitembea katika mji wa Dodoma wakibeba silaha kama panga, mikuki, mishale, rungu, fimbo na hata sime… Ilikuwa kawaida pombe ikinywewa sana, mikuki ilitumika kuwekana sawa. Hivyo kesi nyingi zilitokana na kujeruhi na kuua wakati wa unywaji pombe.
…Anasimulia kuwa siku moja alipokuwa amebakiza siku moja kabla ya kukamilisha kikao cha Mahakama Kuu Tabora, walipata wasi wasi kwa sababu mshtakiwa wa kesi ya mauaji, mashahidi na polisi waliokuwa wanawasindikiza, walikuwa bado hawajafika kwa miguu. Jaji alitakiwa kuwahi treni kwa safari ya Kigoma. Ilitafutwa gari dogo aina ya Ford na akaombwa Hakimu mmoja aitwaye Butler Lloyd afuatilie. Baada ya kuendesha kwa takriban maili ishirini, aliwakuta mshtakiwa wa mauaji akioga mtoni pamoja na polisi, na mashahidi. Mshtakiwa wa kesi ya mauaji na mashahidi katika kesi hiyo walikuwa wamefungwa kwa Kamba wasikimbie, lakini wote walikuwa na furaha ya kuoga na kuondoa
15 | P a g e
uchovu wa kutembea kwa muda mrefu kuelekea Tabora kwa Jaji Mwenye Kanzu Nyekundu. Mshtakiwa na Mashahidi walipandishwa katika gari na kuharakishwa Tabora kwa ajili ya kuwahi kusikilizwa kabla Jaji mwenye kanzu nyekundu hajapanda treni ya kwenda Kigoma."
Mheshimiwa Rais, simulizi za Jaji Alexander zinasaidia kutoa picha ya ulinganifu wapi Mahakama Kuu Dodoma imetoka, hadi kufikia hatua hii ya wananchi kupata huduma za ngazi zote za Mahakama ndani ya Kituo hiki Jumuishi. Safari aliyoanzisha Jaji Alexander kupeleka haki kwa wananchi bado inaendelea na pia ni endelevu. Safari ya Mahakama Kuu kutoka Dar es Salaam aliyoianzisha Jaji Mwenye Kanzu Nyekundu bado haijafika katika mikoa ya Njombe, Geita, Singida, Manyara, Pwani, Katavi, Songwe, Lindi na Simiyu. Mikoa hii bado inasubiri Serikali ya Tanzania unayoiongoza Mheshimiwa Rais, iwezeshe ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu, ili wananchi wapunguziwe umbali wa kutafuta huduma za Mahakama Kuu.
Mheshimwa Rais, Katika ngazi za Wilaya 139 zilizopo Tanzania Bara, Mahakama za Wilaya 20 bado zinasubiri majengo. Ndoto ya Mahakama ya Tanzania ni kila Kata iwe na ngazi ya Mahakama ya Mwanzo, zipo Kata takriban 3,956. Zipo Mahakama za Mwanzo 960 tu, kwa hiyo mahitaji kwa sasa ni Mahakama za Mwanzo 2996. Safari ya kusogeza huduma za utoaji haki bado inaendelea.
16 | P a g e
Mheshimwa Rais, Vituo sita Jumuishi vya Utoaji Haki vimejengwa kwa fedha za wananchi wa Tanzania kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia. Kwa dhati kabisa nichukue fursa hii kuishukuru Serikali unayoingoza kwa kukubali kuchukua dhamana ya mkopo kwa ajili ya kupata fedha zilizotumika kuboresha huduma za Mahakama Tanzania.
Mheshimiwa Rais, ujenzi wa vituo sita vya utoaji haki umegharimu fedha za kitanzania shilingi 51,534,041,969.00 ambapo Dodoma zimetumika 9,297,560,024.00, Arusha 8,293,338,999.00 Morogoro 9,113,440,179.00, Mwanza 8,561,314,505.00, Kinondoni 7,040,671,427.00 na Temeke 9,227,716,835.00.
KWA NINI KITUO JUMUISHI TEMEKE KIWE MAHAKAMA MAALUM KWA KESI ZA KIFAMILIA
Mheshimiwa Rais, Kituo Jumuishi cha Temeke kimebeba dhana kuwa mfumo wa utoaji haki una wajibu wa kuwainua wote miongoni mwa jamii, ambao hawapati nafasi sawa na wengine kupata huduma za utoaji haki. Wanawake, Watoto, Walemavu na watu wanaoishi katika mazingira magumu, wametajwa kuwa hawapati fursa sawa na wengine katika kufikia ngazi za utiaji haki. Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Kutumia Sheria Kuwawezesha Watu Masikini (The United Nations Commission on Legal Empowerment of the Poor (UNDP 2008) inawazungumzia watu hawa.
17 | P a g e
Matumizi ya Sheria na vyombo vya utoaji haki kuwawezesha wasio na fursa sawa, hayatafanikiwa, kama hao Wanawake, Watoto, Walemavu na watu wanaoishi katika mazingira magumu; hawatainuliwa na mifumo ya sheria ili wafikie hiyo mizani ya utoaji haki (Legal empowerment is impossible where the poor, the vulnerable and the marginalized are denied access to a well-functioning justice system).—Sheria itashindwa kuwezesha pale, wananchi walio masikini au katika mazingira hatarishi, watakosa nafasi sawa katika vyombo vya utoaji haki.
Katika historia ya maboresho ya utoaji haki, Kituo Jumuishi cha Temeke kimebeba dhana inayotambua kuwa kwa Wanawake na Watoto bado wana safari ndefu katika kupata haki ya kusikilizwa katika mizani sawa na wananchi wengine, na wanahitaji kurahisishiwa mifumo ya utoaji na upatikanaji wa haki. Kituo Jumuishi cha Temeke kitasogeza huduma kwa wanawake, wajane na watoto katika mashauri ya ndoa, talaka, matunzo, na mirathi. Andiko la mradi wa Benki ya Dunia linatarajia kuwa Vituo Jumuishi na Mahakama zinazotembea (Mobile Courts), zitashirikiana kwa ukaribu katika kuwawezesha VULNERABLE GROUPS kupata haki: “Furthermore, a Justice-on-Wheels (mobile courts) Program will be piloted to empower vulnerable groups (for example, women, youth, and small business) by providing quick and affordable justice services where they live and work.”
Jiji la kibiashara la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na wingi wa mashauri. Mathalani, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa takwimu za Mwezi Septemba 2021 ilikuwa na mashauri zaidi
18 | P a g e
ya 3,000. Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na Mahakama Kuu katika kanda nyingine hapa nchini. Ili kuongeza kasi ya ushughulikiaji wa migogoro Jijini Dar es Salaam, Mahakama ya Tanzania iliamua kujenga vituo viwili Jumuishi vya Utoaji Haki—Kinondoni na Temeke. Aidha, kutokana na unyeti wa mashauri ya Mirathi na Ndoa, Mahakama iliamua Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kimoja kitumike kushughulikia migogoro ya Mirathi na Ndoa. Kituo hicho ni (Temeke One Stop Center), wilayani Temeke.
Uamuzi wa kujenga kituo Jumuishi Temeke ulisukumwa na tatizo la uwepo wa idadi kubwa ya mashauri ya mirathi pamoja na mashauri ya ndoa na talaka. Kwa mfano, kati ya mwaka 2017-2019 kulikuwepo na mashauri 7,600 ya mirathi ambapo kati yake mashauri 3,765 yalikuwa katika ngazi ya mahakama za mwanzo. Mashauri ya ndoa na talaka yalikuwa takribani 4,200 kati ya mwaka 2017-2019. Aidha uhitaji wa kuwa na Mahakama kama hii ni muhimu sana kwa sasa, ambapo maombi mengi ya kuwa na MAHAKAMA MAALUM ya mashauri ya familia, yalitoka katika katika asasi za kiraia na wadau wengine wa haki za binadamu kama Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Chama Cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA). Hawa, kwa nyakati tofauti, waliwasilisha maombi yao kwa uongozi wa Mahakama kuomba ianzishwe Mahakama ya mashauri ya kifamilia.
19 | P a g e
Mheshimiwa Rais, eneo la mashauri ya mirathi, ndilo lina ucheleweshaji mkubwa na malalamiko mengi. Mashauri ya mirathi ni eneo ambalo pia, limekuwa na ulegevu wa upande wetu Mahakama kuwadhibiti wasimamizi wa mirathi ili wafunge mirathi na kuwasilisha mahesabu ya mwisho ya kufunga mirathi mahakamani (inventories)! Mashauri ya mirathi pia yanachangamoto ya wasimamizi wa mirathi kupotosha na kujichukulia kuwa wao ndio wamiliki wa mali zote za mirathi. Kwa ufupi, mashauri ya mirathi yana mianya mingi ya ubadhirifu, wizi, rushwa na kuwanyima warithi (hasa wanawake na watoto) stahiki zao. Mashauri ya mirathi ndiyo yenye nafasi kubwa kwa ndugu, jamaa, familia na ukoo wa marehemu kujadiliana katika vikao na kuafikia makubaliano mapema na kuja Mahakamani ili tu kupata amri ya mwisho tu bila kupoteza miaka mingi katika kesi za mirathi.
Tumejifunza pia vikao vya familia kuamua wasimamizi wa mirathi ndiyo vyanzo vya migogoro inayowasilishwa mahakamani. Moja ya majukumu ya Kituo Jumuishi cha Temeke ni kujenga mifumo ya upatikanaji wa suluhu katika mashauri yanayosajiliwa katika kituo hicho. Temeke iwe chou chetu cha kujifunza namna bora ya kuendesha mashauri ya kifamilia.
Mheshimiwa Rais, uzoefu wetu katika Mahakama umetufundisha kuwa kiasi kikubwa sana cha fedha zinapitia katika taratibu za mirathi na kuwa vyanzo vya migogoro. Kwa wastani, Mahakama imekuwa inalipa kiasi cha TZS 3.8 billioni kwa wasimamizi na warithi wa mirathi kiasi ambacho kinabeba uchumi mkubwa wa
20 | P a g e
wananchi na taifa kwa ujumla. Hivyo, Mahakama iliona ni muda muafaka wa kuimarisha na kuboresha ushughulikiaji na usimamizi wa mashauri ya mirathi kwa kuyapa kipaumbele ili kuhakikisha wananchi na jamii kwa ujumla wanapata huduma na elimu ya usimamizi wa mirathi na utatuzi wa migogoro ya kifamilia kwa ubora na kwa haraka ili wabaki na muda mwingi zaidi kutumia katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo.
Kwa kuzingatia umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, Mahakama ikishirikiana na wadau kupitia BARAZA LA USULUHISHI WA NDOA itatoa huduma hizo katika kituo jumuishi cha kushughulikia migogoro ya Mirathi na Familia -Temeke. Hii ni katika kutekeleza moja ya malengo ya Mpango wa Kuimarisha Mahusiano katika Familia hapa Nchini.
Dhamana Kubwa kwa Watumishi katika Kituo Jumuishi Temeke
Watumishi waliopangiwa kutoa huduma katika kituo Jumuishi cha Temeke (One-Stop-Centre) kumbukeni kuwa mnayo dhamana kubwa. Kituo hiki ni cha mfano katika kushughulikia mashauri ya kifamilia, Watoto, kuhusu ndoa, talaka, matunzo, malezi ya Watoto, mirathi na kadhalika. Ni kituo ambacho majaji, wasajili na mahakimu, watatumia jengo moja pamoja na maafisa ustawi wa jamii, wanasheria wa serikali, mawakili binafsi, watoaji wa misaada ya kisheria, mifuko ya hifadhi ya jamii, huduma za kifedha, watatoa huduma zitakazotegemea ushirikiano wa karibu.
21 | P a g e
Wajibu muhimu wa watumishi katika Kituo Jumuishi Temeke ni kuwasaidia wanandoa, wanafamilia, Watoto, na wote watakaohusika na mashauri waweze kujipanga upya na kuishi maisha mapya mara baada ya kukamilisha shughuli za kimahakama. Hapa naomba kusisitiza utunzaji bora wa kumbukumbu na usiri (confidentiality). Huduma katika kituo cha Temeke zitagusa maswala ambayo kawaida huwa ni siri ya wahusika au inajulikana kwa watu wachache wanaowazunguka.
Waheshimiwa Majaji, Mahakimu na watumishi wote wa umma watakaotoa huduma katika kituo cha Kituo Jumuishi cha Temeke ni lazima wajiongeze kwenye uelewa wa maswala ya KISAIKOLOJIA, SOSHOLOJIA na mbinu za USULUHISHI. Muwe tayari kuwasikiliza wataalamu wengine, kwa mfano, USTAWI WA JAMII, WATAALAMU WA USULUHISHO, WATAALAMU WA MALEZI, WANASAIKOLOJIA na WANATAALUMA WENGINE wenye mchango katika kutatua changamoto zitokanazo na ndoa, talaka, mirathi, watoto na kutenganishwa kwa wanandoa.
Mheshimiwa Rais, tarehe 24 Januari, 2021, wakati kuo ukiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulizindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini na Miaka Mia Moja ya Mahakama Kuu kwenye viwanja vya Nyerere Square hapa jijini Dodoma. Pamoja na kukumbushia umuhimu wa Mahakama kutoa haki kwa wakati, uadilifu, weledi mkubwa, kutoa haki bila upendeleo wala rushwa; ulitukumbusha kuwa, uwepo kwa sheria nzuri peke yake bila NAFSI zetu binafsi kusimama katika mstari wa HAKI, hakutakuwa na hiyo HAKI:
22 | P a g e
“Inasemekana ni nafsi ndio inayoongoza kufanya haki na sio mfumo wa sheria (It is the spirit and not the form of law that keeps the justice) tumia nafsi yako kutoa haki, haki isipelekwe kwa wasio na haki.”
Maneno yako yawe ni sehemu ya utoaji haki katika vituo hivi jumuishi.
Vituo Jumuishi Viwe Vitovu vya Matumizi ya Teknolojia
Mheshimiwa Rais, Jaji Mwenye Kanzu Nyekundu (Jaji Alexander) alikuwa ni Jaji wa Robo ya Kwanza ya Karne ya 20. Alitegemea njia ya reli kupeleka huduma za haki kwa wananchi waliokuwa wakiishi karibu na vituo vya treni. Wananchi walitembea masafa marefu ili wafikie vituo vya utoaji haki. Mheshimiwa Rais leo unapozindua Vituo Jumuishi tupo Robo ya Kwanza ya Karne ya 21 inayotegemea matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kufanikisha utoaji haki.
Mheshimiwa Rais, hakuna mtumishi wa Mahakama ambaye hatambui ufanisi na weledi mkubwa ambao Mahakama ya Tanzania imepata baada ya kufanya uwekezaji mkubwa katika mifumo na matumizi ya teknlojia chini ya mradi wa maboresho ya Mahakama. Vituo Jumuishi ni lazima viwe chachu ya safari ya kufikia Mahakama Mtandao ya Karne ya 21, ambayo itamrahisishia mwananchi upatikanaji wa huduma bora za kimahakama kwa wakati. Ufanisi na weledi wa watumishi watakaohudumu Vituo Jumuishi utapimwa kwa kuzingatia
23 | P a g e
kiwango cha matumizi ya teknolojia na TEHAMA kuwezesha kuwafikishia wananchi huduma za utoaji haki.
Mheshimiwa Rais, Mahakama ya Karne hii ya 21 inategemea barabara ya MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO na upatikanaji wa huduma za mtandao “Internet” ili kuwafikishia wananchi huduma za utoaji haki. Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya hazitegemei tena njia ya reli, bali zimeunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL). Zinatumia huduma ya Internet katika usikilizaji wa mashauri na utoaji wa taarifa za mashauri. Kadri Serikali unayoiongoza itakavyosambaza huduma za Internet zenye gharama nafuu, hivyo hivyo, huduma za Mahakama Mtandao zitawafikia wananchi wengi zaidi.
Tunawaomba Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) waichulie Mahakama ya Tanzania kama Zaidi ya mdau/mteja wake muhimu. TTCL ichukuliwe kuwa mtoa huduma za utoaji haki katika kusaidia kuyafikia Malengo Matano katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Shirika (TTCL) likiboresha huduma za Internet pamoja na kuitoa kwa gharama nafuu, zitaipunguzia Mahakama mzigo mkubwa wa gharama za malipo ya mtandao “Internet” unaobebwa kwa sasa.
24 | P a g e
MWISHO
Mheshimiwa Rais, Kwa mara nyingine tena tunapenda kukushukuru sana kwa jitihada zako binafsi na za Serikali kwa kutuwezesha na kuendelea kutuwezesha ili tufanikiwe katika lengo letu la kuboresha huduma za Mahakama. Nimshukuru pia Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia ndugu Mara Warwick kwa niaba ya Benki hiyo ambao wametoa mchango mkubwa katika maboresho ya Mahakama ya Tanzania ambayo yanakamilisha awamu ya kwanza ya miaka mitano na kujitayarisha kwa miaka mitano ya pili ya maboresho. Shukrani za pekee pia ziende kwa wadau wetu wote ambao tunashirikiana nao kuwafikia wananchi. Shukrani ziende kwa vyombo vyote vya habari ambavyo kwa hakika vimekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu maboresho ya Mahakama. Niwahakikishie kwamba Mahakama itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote na vyombo vyote vya Habari.
Mheshimiwa Rais, baada ya kusema haya, kwa heshima na taadhima, nakukaribisha uongee nasi, utupe nasaha zako, ukizingatia kuwa utakuwa pia unaongea na Watanzania wote kupitia vyombo vya Habari. Mhe. Rais KARIBU SANA!
Asanteni kwa kunisikiliza.