Hotuba fupi ya mheshimiwa jaji mkuu katika hafla ya kuwaapisha mahakimu wakazi wapya 39 TRH 27/11/2020

- Mhe. Jaji Kiongozi,
- Mhe. Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam,
- Mhe. Mtendaji Mkuu wa Mahakama
- Mhe. Kaimu Msajili Mkuu,
- Mhe. Msajili Mahakama Kuu
- Wah. Naibu Wasajili,
- Wah. Mahakimu Wafawidhi,
- Watendaji na watumishi wa mahakama mliopo
- Familia ya Mahakimu wapya
- Salaaam
Napenda kuchukua nafasi hii kwa moyo wa dhati kabisa kumshukuru Mungu na kuwakaribisha Mahakimu wote wapya katika Utumishi wa Mahakama ya Tanzania. Karibuni sana.
Kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania nawashukuru sana viongozi, familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopata nafasi ya kuja kujumuika nasi katika kushuhudia Mahakimu wapya wakiapa/kuthibitisha kabla ya kuanza utumishi wa Mahakama katika nafasi ya Uhakimu DARAJA LA II.
MAJUKUMU YA HAKIMU NI YA KIKATIBA
Wakati wa kiapo/uthibitisho wenu, muliapa kwa kuinuia Katiba ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania.
Ishara hii ina umuhimu wa kipekee. Hii kwa sababu mamlaka na madaraka yenu yamepewa umuhimu na uzito wa Kikatiba, na mnaelekezwa na Ibara ya 107A (2) kuwa katika Kutoa maamuzi ya mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, mtaongozwa na kanuni zifuatazo:
- Kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi;
- Kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi;
- Kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine, na kwa mujibu wa sheria mahsusi iliotungwa na Bunge;
- Kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro; na
- Kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi anaoweza kukwamisha haki kutendeka.
Hii ni ahadi ambayo lazima muibebe siku zote.
Katiba yetu, kwa mujibu wa Ibara ya 107B, imewahakikishieni nyie Mahakimu (Pamoja pia na Wasajili, Majaji) kuwa, katika kutimiza ahadi ya viapo/vithibitisho vyenu-
“Mtatekeleza mamlaka ya utoaji haki, kupitia Mahakama zitakazokuwa huru na mtalazimika kuzingatia tu, masharti ya Katiba na yale ya sheria za Nchi.”
Maana yake ni kwamba, muongozwe na Katiba, Sheria na taratibu za kimahakama katika kazi zenu za Uhakimu.
Adui mkubwa wa Uhuru wako wewe Hakimu, ni endapo itaonekana kuwa Shahada yako ya Sheria, uliopata/chuo Kikuu, na Ufaulu wako katika Shule ya Sheria kwa Vitendo, havilingani na ubora unaotarajiwa kutoka katika kazi zako kama HAKIMU, na hazilingani na tabia na mwenendo mzuri unaotarajiwa kutoka kwa HAKIMU. Kila siku kazi yako ya Uhakimu, itapimwa kama kweli ni linganifu na vyeti vyako.
Uhakimu wako utaimarika endapo siku zote utazingatia SHERIA, na kuongozwa na TARATIBU, KANUNI na NYARAKA zinazotolewa mara kwa mara na viongozi wa Mahakama.
Kazi ya uhakimu sio kazi ya kuchukuliwa kimazoea au kwa wepesi wepesi. Hata kwa baadhi yenu, ambao mlikuwa watumishi wa Mahakama kama Makarani, watunza kumbukumbu, wahudumu na madereva; kazi ya Uhakimu ni mpya kwenu.
Kila mmoja wenu atagundua hivi karibuni kuwa SIKU YAKO YA KWANZA KUINGIA MAHAKAMANI ukiwa na HADHI YA UHAKIMU,
haitakuwa siku ya majaribio kwa sababu kila Uamuzi utakaoutoa hiyo SIKU YAKO YA KWANZA hautakuwa wa majaribio.
Bali, uamuzi wako utagusa UHAI, MALI na HALI ya wanadamu wengine na watanzania. Kosa lolote la kimaamuzi mtakalotoa siku ya kwanza na siku zifuatazo, litakuwa na faida au hasara kwa Nchi, kwa watu, kwa familia na kadhalika.
Hatutegemei MAHAKIMU kufanya MAKOSA, hasa katika maeneo ambayo sheria iko wazi; kwa sababu HAKIMU anatakiwa kujitayarisha sana (kuelewa sheria na taratibu zote za shauri lililo mbele yake kabla ya kuingia Mahakamani).
Siku zote kumbukeni kuwa, Makosa ya Hakimu yanaweza kusababisha wahalifu, kwa mfano wa madawa ya kulevya, wezi, wanyang’anyi, wabakaji kurudi kwenye jamiii na sio tu kuendeleza uhalifu bali pia kuwapa moyo wahalifu wengine kuwa unaweza kufanya uhalifu lakini mahakama ikafanya kosa la kuwaachia huru. Hata kama nafasi ya rufani ipo, kwa aliyefungwa kimakosa- makosa yanaweza kurekebishwa kupitia rufani baada ya miaka hata ishirini baada ya kosa la Hakimu.
Hivyo hivyo, makosa ya Hakimu yanaweza kumtia hatiani mwananchi ambaye hajatenda kosa. Makosa yataepukika endapo Mahakimu watajisomea MAAMUZI YA Mahakama Kuu, ya
Mahakama ya Rufani ambayo yanapatikana kwa urahisi kabisa katika Tovuti ya Mahakama (TANZLII). Ni kosa kubwa sana kwa Hakimu, ambaye hatasoma maamuzi ya Mahakama ya juu kuhusu mambo yanayogusa kazi za Hakimu.
Mbali na Katiba, nyaraka nyingine mliyokabidhiwa leo hii ni KANUNI ZA MAADILI ZA MAAFISA MAHAKAMA (CODE OF CONDUCT AND ETHICS FOR JUDICIAL OFFICERS, 2020). KANUNI
hizi zilipitishwa na TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA na kusainiwa tarehe 21/10/2020.
KANUNI HIZI sio mapambo kwa shughuli za leo na baada ya shughuli kila mtu atazisahau! Ni Kanuni zinazotoa miongozo muhimu katika kazi za kila siku za Uhakimu.
Utangulizi (Preamble) wa kanuni za maadili za maafisa mahakama unawakumbusha nafasi ya Mhimili wa Mahakama katika muktadha wa Tanzania (social-economic context) kwa kutamka kuwa Mahakama iliyo huru, iliyo imara na inayoheshimika kwa kutoa haki bila upendeleo haiepukiki kama nchi inataka kujenga Taifa la kidemokrasia.
Hivyo basi, uhuru wenu katika maamuzi, ni maagizo ya kujenga demokrasia na utawala wa sheria. Uhuru wa Mahakama na Uhuru wa Hakimu ni kwa faida ya Nchi kwa ujumla, na sio kwa faida au utashi wa Hakimu au Jaji husika.
Utangulizi (Preamble) wa kanuni za maadili za maafisa mahakama umesisitiza kwamba; Imani ya wananchi kwa Mahakama inatokana na utendaji wenu wa kazi za Uhakimu. Kumbukeni, Mahakama za Mwanzo hubeba asilimia 70 ya kesi zote zinazosajiliwa na kusikilizwa katika Mahakama za Tanzania.
Kama mtatoa haki kwa kuzingatia misingi ya haki, bila woga wala upendeleo, na kwa kufuata Sheria; basi Imani ya wananchi wengi itaongezeka. Kanuni hizi za Maadili zinasisitiza kuwa Majaji, Wasajili, Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama hawako juu ya Sheria na wamewekewa mifumo ya uwajibikaji.
Ili kulinda uhuru wenu wa kusikiliza na kutoa maamuzi, Kanuni za Maadili zimewaagiza, kuonyesha kwa vitendo na mifano uhuru wenu, msikubali wala kuendekeza vishawishi vya aina yoyote kutoka ndani ya mahakama au kutoka nje ya Mahakama vitakavyo jaribu kuingilia maamuzi yenu.
Chungeni sana simu zenu za mkononi maana hizi zinaweza kutumika kuingilia uhuru wenu katika kufikia maamuzi yenu. Kwa ufupi, usipokee shinikizo kupitia simu za mkononi.
Vishawishi visivyotakiwa vinaweza kutoka kwa ndugu, familia, marafiki, majirani, kiongozi wa kiroho na kadhalika. Hivyo basi, ni lazima muangalie upya ZAWADI mbali mbali kutoka marafiki, MISAADA, MAHUSIANO, wapi mnatembelea, makundi gani ya starehe au mapumziko mnayoshiriki pamoja na hata picha
angalieni mnapiga picha nan nani. Aidha tambueni SHINIKIZO au USHAWISHI usiotakiwa unaweza kukufikia kupitia makundi ya kijamii (Social media, WHATSAPP, FACEBOOK, INSTAGRAM).
Yapo malalamiko ya Mahakimu kutembelewa katika ofisi zao na marafiki, ndugu, jamaa au watu wakati wakijitayarisha kuanza mashauri. Hili halikubaliki. Wageni wote waache shida zao kwa Hakimu Mfawidhi au Watendaji wa Mahakama. Usiruhusu mtu yeyote kuja katika (Chambers) ofisi yako bila kupata ridhaa ya Mfawidhi wako.
Uadilifu (Integrity)
Unaweza kuwa HAKIMU unayefahamu sana Sheria na taratibu za kisheria nan za kimahakama. Lakini, bila uadilifu, umahiri wako unaweza kutumika kuzorotesha au kupoteza haki halali za wengine. Suala la uadilifu limepewa uzito mkubwa katika kanuni za maadili za maafisa mahakama (Code of Conduct and Ethics For Judicial Officers, 2020).
Tabia zako ukiwa mbele ya umma au ukiwa katika maeneo yasiyo ya umma, lazima yasitiliwe mashaka na watu wa kawaida na yasaidie kuimarisha Imani ya wananchi kwako kama HAKIMU na kwa Mahakama kwa ujumla.
Baadhi ya Maafisa wa Mahakama wana kawaida ya kujiunga katika makundi ya mitandao ya kijamii. Wengine wanatumia majina ya bandia katika mitandao ya kijamii kushiriki katika majadiliano,
ambayo mengine hayaendani na maadili ya Maafisa Mahakama. Hili halikubaliki. Unaweza kuhusishwa na kinachojadiliwa katika kundi lako hata kama wewe binafsi hujachangia chochote.
Usikubali upendeleo (favours), kama zawadi, au nafuu au mkopo wenye masharti nafuu, kiasi cha kuonekana kuwa ni rushwa iliyofichwa. Masharti ya uadilifu yamewakataza kutoa ushauri wa kisheria kwa watu wengine isipokuwa kwa ndugu zako.
Ni kosa kubwa la kimaadili endapo kwa mfano, ukirudi nyumbani jioni, wakili wa kujitegemea au kampuni ya Uwakili au mwananchi mwenye kesi Mahakamani, anakuja kukuomba ushauri au anakuletea majalada ya kesi ili uwasaidie kutoa maoni au hata kuwataarishia nyaraka za kisheria ili wao waweke majina nan Saini zao.
Uwezo wa kufanya kazi za Hakimu
Uongozi wa Mahakama na Tume ya Utumishi wa Mahakama wana amini kuwa kila mmoja wenu anao uwezo wa kufanya kazi za Hakimu. Kanuni za maadili za maafisa mahakama zimetoa msisitizo maalum kwa suala la “Competence and Diligence” yaani Uwezo wa kufanya kazi za utoaji haki, umahiri katika kazi ya utoaji haki, bidii na umakini wa kufanya kazi za kimahakama.
Maana yake ni kwamba, unaweza kuondolewa katika kazi ya Uhakimu kwa kushindwa kufanya kazi, kutokana na sababu mbali mbali kama—uvivu, ucheleshwaji wa maamuzi, kuchelewa kazini
na kadhalika. Kila hukumu mtakayoandika itapitiwa na wataalamu wa Mahakama ili kuwapima na kuwapa mrejesho kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa. Hii ni kuhakikisha uwezo wenu unazidi kuongezeka siku hadi siku.
HAKIMU lazima ajisomee, sio tu mambo ya kisheria bali pia mambo mengine ya kuwawezesha kuifahamu Tanzania, changamoto zinazoikabili Tanzania na matatizo mbali mbali yanayowakabili watanzania. Hakimu lazima ajisomee kwa kufuatilia mabadiliko ya sheria na kutumia TEHAMA kuboresha kazi zake.
MAHAKAMA BADO HAIZUNGUMZWI VIZURI KUHUSU RUSHWA KIMTAZAMO KUTOKA NJE YA MAHAKAMA (PERCEPTION):
Mahakama ya Tanzania imejiweka utaratibu wa kupima inavyotazamwa (perceived), kwa namna gani wananchi wa kawaida wanaona huduma za utoaji haki za Mahakama. REPOA walifanya utafiti huo mwaka 2015 na pia 2019 ripoti za utafiti zimesaidia Mahakama kufahamu wananchi wanaitazamaje Mahakama na huduma za utoaji haki.
Vitendo vya rushwa bado vipo, na bado vinatushushia heshima mbele ya UMMA. Taarifa ya Jaji Kiongozi ya hivi karibuni inaonyesha kuwa hadi tarehe 20 ya Mwezi huu wa Novemba 2020, kati ya kesi NANE (8) za jinai zinazowakabili Mahakimu Mahakamani, kesi SABA (7) ni tuhuma za KUDAI NA KUPOKEA RUSHWA. Sio picha nzuri hata kama kuna kesi moja tu, dhidi ya HAKIMU - bado ni doa.
Ni fedheha, kwa MHESHIMIWA HAKIMU, kufikishwa Mahakamani mbele ya hakimu mwenzake akituhumiwa kudai na kupokea rushwa.
RUSHWA ina tabia ya kujificha, ipo lakini haizungumzwi, na haijionyeshi wazi wazi. RUSHWA isiyojionyesha inaweza kuondolewa kwa haraka kama watumishi wa Mahakamani wataizungumzia na kuikemea bila kusubiri taasisi za nje ya Mhimili wa Mahakama (kwa mfano TAKUKURU) kuingilia kati.
Tume ya Rushwa ya Jaji Warioba ya Mwaka 1996 ilibainisha maeneo yanayotoa vipenyo kwa vitendo vya rushwa kushamiri kwa kificho ndani ya Mahakama. Tujihadhari na vipenyo hivyo hatarishi kwa kuruhusu RUSHWA, kwa mfano:
- Wakati wa kufungua mashauri
- Wakati wa kupanga tarehe za kesi
- Wakati wa kutafuta majalada ambayo yanadaiwa kuwa hayaonekani
- Wakati wa kupata nakala za hukumu
- Wakati wa kutoa dhamana katika kesi za jinai
- Wakati wa kutoa amri za zuio kwa faida ya wasiostahili
- Washtakiwa waliotiwa hatiani kutoa rushwa kwa hakimu ili asitoe adhabu za vifungo na badala yake Hakimu atoe adhabu ya faini.
MAHAKAMA BADO HAIZUNGUMZWI NA KUTAZAMWA VIZURI KUHUSU UCHELEWESHWAJI WA MAAMUZI
Mahakama za Mwanzo mtakapoanzia kazi hazina kabisa tatizo la ucheleweshwaji wa mashauri kwa sababu Mahakama za Mwanzo zinaweza kumaliza mashauri ndani ya miezi sita. Isipokuwa, katika eneo la mirathi bado kuna ucheleweshwaji.
Mahakama nyingi zinakiuka sheria kwa kutotekeleza masharti ya Usimamizi wa mirathi kwa kushindwa kuhakikisha kuwa majalada ya mirathi yanafungwa kwa wasimamizi kuwasilisha MAHESABU YA MWISHO KUHUSU MALI, MADENI NA MGAWANYO
(INVENTORY) ndani ya miezi 6. Mahakama zimejilegeza kiasi cha kuwaachia Wasimamizi wa Mirathi watumie vibaya mali za marehemu pamoja na hata kupora mali yote. Fuateni utaratibu mwepesi wa kisheria.
Eneo lingine ambalo wananchi wanalalamika sana, na wanayo sababu za kulalamika hasa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi—ni ucheleweshwaji mkubwa wa kesi kubwa kubwa za mauaji, madawa ya kulevya, nyara za serikali, uhujumu uchumi, ugaidi, utakatishaji wa fedha.
Mahakimu wanafanya kosa kubwa la kukubali Maahirisho yasio na kikomo na bila kupokea sababu zozote, sababu kuwa UPELELEZI UNAENDELEA SIO SABABU. Wananchi wanatuambia kuwa, waendesha mashtaka wanatumia ucheleweshaji Mahakamani kama adhabu kabla hata kosa halijathibitishwa Mahakamani.
Ili kuziba mwanya uliokuwa unatumiwa na waendesha Mashtaka na wapelelezi wa kuomba maahirisho yasio na kikomo, Mhe. Jaji Kiongozi alitoa WARAKA NAMBA 5 WA 2019 kuhusu KUHARAKISHA Committal Proceedings, Plea Taking na Preliminary Hearing. Waraka huu aliuelekeza kwa Waheshimiwa Majaji Wafawidhi na Mahakimu Wafawidhi akiwaagiza:
- RMs in-Charge of committing courts to ensure committal proceedings are conducted and finalized within two weeks from the date of receiving the information and its annexures from Deputy Registrars in respect of High Court Zones;
- Ensure committal proceedings records are typed, compiled and served to parties in terms of section 249 of the CPA followed by remittances of court record to the High Court within two weeks from the conclusion of committal proceedings unless extension is applied for and granted by the Judge in-Charge. This means committing courts should conduct and finally remit the committal proceedings record to the High Court within thirty days. Ensure case files are assigned to Judges or Magistrates with Extended Jurisdiction within two weeks after their remittance to the High Court Registry for purposes of allowing adequate preparations by the parties to the cases.
- Ensuring that plea and Preliminary Hearing are taken and conducted within two weeks from the date of assignment of the case files.
- Ensuring that Deputy Registrars at all time maintains adequate and effective communication with stakeholders like Prison Officers in-charge of District or Regional Prisons where remand prisoners are kept; District or Regional Prosecution Officers in-charge and assigned legal representatives from the TLS or appointed by the accused.
Ucheleweshwaji mkubwa wa kesi kubwa kubwa kamwe hautokani na mapungufu ya sheria, bali ni mapungufu yetu sisi Majaji, Wasajili na Mahakimu. Hatujawawajibisha waendesha mashtaka. Hakimu mwenye uwezo na maadili hana sababu ya kumhofia Mwendesha mashtaka. Tumieni mamlaka na madaraka yenu kwa faida ya wananchi ambao kesi zao za jinai zinaahirishwa bila kikomo.
Kuna hatua kadhaa ambazo Uongozi wa Mahakama umezichukua kuhakikisha kuwa WARAKA WA JAJI KIONGOZI unatekelezwa ili kusukuma usikilizwaji wa kesi kubwa kubwa za jinai:
- Kitengo cha TEHAMA kitaweka utaratibu wa kufuatilia ki- elektroniki mtiririko wa kesi kubwa zote za jinai zinazokwama katika hatua za Mahakimu na kujua ni HAKIMU yupi ameshindwa kutumia mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa Waraka wa Jaji Kiongozi;
- Tutawapeleka Mahakimu wote ambao wanakiuka mtiririko wa muda uliowekwa na WARAKA wa JK mbele ya Kamati ya Maadili kwa tuhuma ya kupoteza sifa ya uwezo (competence)
wa kufanya kazi za HAKIMU na baadae TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA itoe maamuzi.
Yapo maamuzi mengi ya Mahakama ya Rufani yanayokataza ucheleweshwaji wa kesi, ambao siku hizi imekuwa jambo kama limekubalika na kuzoeleka. Mahakimu wengi siku hizi muda wao mwingi ni kuahirisha kesi badala ya kusikiliza. Huu sio utaratibu unaozingatia misingi ya HAKI na haukubaliki.
Katika kesi ya IBRAHIM SAID MSABAHA VS. LUTTER SYMPHORIAN NELSON & AG, CIVIL APPEAL NO. 4 OF 1997, NYALALI CJ:
“We think that the approach of this court which seeks to discourage adjournments of cases on flimsy or no grounds at all should be followed by all courts in this country, not only because delay amounts to a denial of justice, but also because it is common knowledge that there is widespread outcry by the people of this country against unnecessary and rampant adjournments of cases by courts. We do emphasize the point that the discretion of a court to adjourn a case which is scheduled for hearing must always be exercised judicially, that is, for good cause which must be recorded.”
Niwakumbushe Mahakimu wapya ucheleweshwaji wa mashauri na maahirisho yasio na sababu nzuri, ni uvunjifu wa HAKI na sio
utamaduni wa Mahakama unaongozwa na misingi ya Katiba na Sheria.
Kuweni Sehemu ya Maboresho ya Mahakama
Katika karne hii ya 21 yenye kusukumwa na ushindani na matumizi ya TEHAMA, pamoja na kusikiliza mashauri kama Mahakimu, mtawajibika kuwa sehemu ya programu za maboresho na mtapangiwa kazi za ziada za kimkakati. Mahakimu ni sehemu ya utekelezaji wa MPANGO MKAKATI na PROGRAMU ZA MABORESHO.
Laptops
Kwa kutambua kuwa utoaji wa haki katika karne hii ya 21 yenye ushindani mkubwa nimeambiwa kuwa kila mmoja wenu atapewa LAPTOP. Hii itawasaidia kutekeleza kwa vitendo lengo la Mahakama la kutoa nakala za hukumu mara baada ya kusomwa na si Zaidi ya siku 21 baada ya kusomwa.
Heshimuni Kazi ya Uhakimu
Wananchi watawaita “Waheshimiwa”. Hii ina maana pamoja na kwamba unaheshimiwa, utajiheshimu, utawaheshimu binadamu wote utakaokutana nao, na utaiheshimu kazi ya Uhakimu. Nyote mnatambua ushindani mkubwa mliopitia hadi kupata kazi za Uhakimu. Mtakumbuka kuwa Tume ya Utumishi ya Mahakama ilitangaza nafasi 114 za Ajira ya Mahakimu Daraja la Pili (II).
Walioomba walikuwa 1,296. Walioitwa usaili walikuwa 342. Miongoni mwenu ni Mahakimu 18 ambao kati ya 114, taratibu zenu za ajira zimekamilika na ndio sababu ya kuapishwa leo kama Mahakimu Wakazi Daraja la II na mtaanzia Mahakama za Mwanzo.
Miongoni mwenu pia wapo Mahakimu wengine 21 walioapa leo, ambao walikuwa watumishi wa Mahakama katika kada zingine ambao, baada ya kujiendeleza na kupata sifa, wamebadilishwa kuwa Mahakimu Daraja la II. Pamoja na kupata Sifa baada ya kujiendeleza, Tume ya Utumishi wa Mahakama iliagiza mfanyiwe usaili kwa lengo la kupima uwezo wenu. Nawapongeza kwa kufaulu huo usaili.
Mahakimu 21 waliojiendeleza, ni kielelezo kizuri kwa watumishi wa Mahakama kupewa nafasi ya kujiendeleza na kubadilishiwa kazi. Kuweni Mahakimu wa mfano kwa wengine ambao bado wapo katika hatua za kujiendeleza.
Ni matumaini ya Tume ya Utumishi ya Mahakama na pia Uongozi wa Mahakama, kuwa makundi yote haya mawili ya MAHAKIMU ni bora na mtakuwa na msaada mkubwa katika utoaji wa haki bora kwa wakati kuanzia katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo; na mkionesha uwezo na maadili mtapandishwa kwenda Mahakama za Wilaya.
Wafundisheni Wananchi Kuhusu Taratibu za Kimahakama
Kwa mujibu wa malalamiko yanayopokelewa katika ofisi ya Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi, inathibitika wananchi walio wengi hawajui haki zao, na pia hawajui taratibu za kimahakama. Kwa kuwa Mawakili hawaruhusiwi katika Mahakama za Mwanzo, Mahakimu wa mahakama za Mwanzo mna wajibu wa kuwasaidia wananchi waelewe taratibu, kanuni, utaratibu na mtiririko wa hatua za mashauri mahakamani.
Hivyo tunategemea wewe Hakimu kama kiongozi kuwa mfano wa kuwaelimisha wadaawa juu ya haki za waadawaa bila kuathiri kiapo chako na bila kufanya kazi ya uwakili kwa faida ya upande mmoja.
Mwisho kabisa nawatakia kila la heri katika majukumu yenu mapya ya Uhakimu. Nimeambiwa kuwa baada ya kuapishwa mtapata mafunzo ya siku tano katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Hayo mafunzo ni hatua muhimu sana katika kazi zenu za Uhakimu. Nawatakiwa safari njema mnapoelekea katika mafunzo hayo huko Lushoto, mafunzo haya yatawasaidia kutekekeza majukumu yenu katika vituo vyenu vya kazi mlivyopangiwa.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA